FAO in Tanzania

Wanafunzi wabunifu wa kibanda bora cha mama/baba lishe wapongezwa

Mmoja wa Wanafunzi akitoa maelezo juu ya kibanda hicho
16/08/2020

Wanafunzi kumi kutoka katika vyuo vya elimu ya juu hapa nchini wamepongezwa kwa ubunifu wao wa kutengeneza kibanda bora na cha bei nafuu kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wa chakula maarufu kama ‘Mama/Baba Lishe’ chenye kuzingatia usafi na usalama wa chakula ili kulinda afya za walaji.

Pongezi hizo zimetolewa na  Kaimu Katibu Tawala Uchumi na Uzalishaji, Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Elizabeth F. Mshote ambaye aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Rashid Mfaume katika hafla fupi ya kutoa zawadi na vyeti kwa washiriki wa shindano la ubunifu wa kutengeneza ‘kiosk’ hicho cha gharama nafuu kitakachotumika na mama/baba lishe jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo ilifanyika katika Ofisi za Asasi ya COUNSENUTH, Mikocheni Dar es Salaam.

Mchango wa Wasomi kwa Jamii

“Napenda kuwapogeza washiriki wote kwa ubunifu huu wa hali ya juu. Huu ndio mchango wa mfano wa wasomi kwa jamii. Suala la usafi na usalama wa chakula ni jambo muhimu sana katika kulinda afya ya umma. Hivyo nanyi mmechangia katika kufanikisha hilo,” alisema. Katika hafla hiyo fupi Dkt. Mshote pia alizindua kibanda hicho kinachotarajiwa kuleta manufaa makubwa na kuboresha biashara ya wauza vyakula wadogo kwa kuboresha huduma zinazotolewa na kuwezesha wateja wao kula mlo kamili ulio safi na salama na hatimaye kuwa na afya njema.

Mchakato huu wa ubunifu na uandaaji wa kibanda cha bei nafuu ulisimamiwa na Asasi ya COUNSENUTH kwa niaba ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa ushirikiano na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, na uongozi wa jiji la Dar es Salaam ambapo ulihusisha mashindano ya wanafunzi kutoka vyuo vya elimu ya juu vya masomo ya usanifu, ujenzi wa majengo/majenzi kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi (Dar es Salaam), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya. Washindi wawili wa shindano hili walisimamia ubunifu na utengenezaji wa kioski hiki chenye kuzingatia masuala ya usafi na usalama wa chakula. Shindano hili lilikuwa sehemu ya ‘Mradi wa Kuboresha Biashara za Mama/Baba Lishe kwa Ukuaji wa Uchumi Dar es Salaam’ unaofadhiliwa na FAO na kutekelezwa katika halmashauri zote tano za Jiji la Dar es Salaam na Asasi ya COUNSENUTH kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Utafiti wa FAO

Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Mchambuzi wa Masuala ya Usalama wa Chakula na Lishe wa FAO kwa hapa Tanzania, Fadhili Mtengela, alisema kuwa mradi huu unafuatia utafiti uliofanywa na FAO ambao uligundua changamoto mbalimbali zinazowakabili Mama/Baba lishe katika Mkoa wa Dar es Salaam. “Mradi huu unalenga kuwajengea uwezo Mama/Baba lishe ili waweze kuboresha huduma wanazotoa kwa kuzingatia usafi na usalama na hivyo kuchangia katika kulinda afya ya umma ikizingatiwa kuwa wakazi wengi wa mijini wanategemea sana huduma zao,” alisema. Alibainisha kuwa lengo ni kuwajengea uwezo Mama/Baba lishe ili waweze kuboresha huduma wanazotoa, hususan kuboresha usafi na usalama na kwamba pia walijengewa uwezo wa kutayarisha vyakula ambavyo vina ubora kilishe, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanatayarisha chakula ambacho ni mlo kamili.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa COUNSENUTH, Dr. Lunna Kyungu alisema COUNSENUTH ilipewa jukumu na FAO la kusimamia eneo la utaalam katika mradi huo kwa kushirikiana na Serikali pamoja na taasisi zake ikiwemo Wizara ya Afya pamoja na wadau wengine.

“Sisi kama wadau muhimu katika mradi huu tuna furaha kubwa kuona jinsi gani wanafunzi hawa walijitoa katika kubuni na kutengeneza kibanda hiki ambacho kitatumika kama mfano wa ujenzi wa vibanda vingine vingi vya namna hii kwa jiji zima la Dar es Salaam lengo likiwa ni kulinda afya ya umma,” alisema.