FAO in Tanzania

FAO, Serikali kushirikiana kuboresha mfumo wa uchambuzi wa masuala ya wa usalama wa chakula nchini

Mkurugenzi wa Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe akizungumzwa wakati wa uzinduzi wa Mradi wa kuboresha Mfumo wa Uchambuzi wa Masuala ya Usalama wa Chakula na Lishe Nchini
22/01/2019

Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) imezindua mradi maalum unaolenga kuboresha Mfumo wa Uchambuzi wa Masuala ya Usalama wa Chakula na Lishe Nchini (MUCHALI).

Uzinduzi wa mradi huu ulifanyika jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Maafa - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kanali Jimmy Matamwe, na Shirika la FAO liliwakilishwa na Ofisa Mtaalam wa Masuala ya Lishe wa FAO, Bi. Stella Kimambo.

Mkazo kwenye usalama wa chakula na lishe

Akizungumza muda mfupi kabla ya uzinduzi, Col. Matamwe alisema kuwa serikali inatilia mkazo mkubwa katika masuala la usalama wa chakula na lishe hapa nchini ili kuhakikisha wananchi wote wanapata chakula cha kutosha na chenye virutubisho vyote muhimu muda wote.

“Suala la ukosefu wa lishe bado ni tatizo nchini, mamilioni ya watu hususan kundi la kaya lenye kipato cha chini wako kwenye hatari kubwa zaidi,” alisema na kuongeza “Katika kuhakikisha usalama wa chakula na lishe inahitajika ufuatiliaji wa mara kwa mara na kuchukua maamuzi stahiki katika utekelezaji wa  jukumu la hali endelevu ya usalama wa chakula na lishe nchini.”

Mfumo wa MUCHALI unazingatia mihimili minne ya usalama wa chakula ambayo ni upatikanaji, Ufikiwaji  wa Chakula, utumiaji na ulaji wa chakula na uhakika wa upatikanaji.

Col. Matamwe alisema kuwa kupitia mradi huu, mfumo wa tathmini na uchambuzi wa masuala ya usalama wa chakula na lishe utaboreshwa kuanzia ngazi ya wilaya pamoja na uboreshwaji wa ukusanyaji wa taarifa kwa kutumia technolojia ya simu hivyo kusaidia  upatikanaji wa takwimu na taarifa husika kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya Serikali na wadau mbalimbali.

Umuhimu wa taarifa sahihi katika kufanya maamuzi

Kwa upande wake Bi. Kimambo alisema kuwa FAO inayo furaha kubwa kushirikiana na Serikali kupitia wataalam wa uchambuzi wa masuala ya usalama wa chakula na lishe ili kuboresha mfumo huo utakaohakikisha upatikanaji wa takwimu na taarifa za masuala ya chakula na lishe kwa wakati, zenye ubora na zakuaminika.

“Watoa maamuzi wanahitaji taarifa zilizo bora, za kuaminika na kwa wakati ili kutatua changomoto ya ukosefu wa chakula na lishe mapema kabla ya madhara yake kuwa makubwa na kuathiri watu wengi,” alisema. 

Katika kutekeleza mradi huu mafunzo yatatolewa kwa wataalam sabini na nane kutoka katika timu za MUCHALI kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Ofisi ya Waziri Mkuu- Idara ya Maafa, Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Taasisi ya Chakula na Lishe, Chuo Kikuu Dodoma, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula,  Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Wengine watatoka Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi (Zanzibar) pamoja na wadau wa kimataifa wa maendeleo kama vile Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa na Msalama Mwekundu.