FAO.org

Home > Country_collector > FAO in Tanzania > News > Detail
FAO in Tanzania

Elimu ya Misitu ni Muhimu kwa Misitu Endelevu

01/04/2019

Na Fred Kafeero *

Misitu ni muhimu sana kwani maisha yote juu ya dunia, ikijumuisha uhai wetu, yanaitegemea. Inatoa vipato kwa wanadamu, ni sehemu ya makazi kwa wanyama, inalinda vyanzo vya maji; inazuia mmomonyoko wa udongo; na inasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo, pamoja na umuhimu huu wote, misitu inaendelea kutoweka kwa kasi ya ajabu ulimwenguni pote! Kwa mujibu wa Taarifa ya Tathimini ya Misitu Duniani ya mwaka 2015, mwaka 1990 dunia ilikuwa na hekta milioni 4,128 za misitu lakini ilipofikia mwaka 2015 ilipungua mpaka hekta milioni 3,999. Kuna sababu nyingi zinazotolewa zikijumuisha ongezeko la watu; upanuzi wa ardhi kwa ajili kilimo; matumizi ya kuni kama chanzo cha nishati pamoja na matumizi mengine ya ardhi yasiyo zingatia faida endelevu. Hapa nyumbani Tanzania, Ripoti ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Rasilimali za Misitu ya mwaka 2015, ilikadiria kuwa kiwango cha ukataji misitu kwa mwaka kilikuwa hekta 372,816, wakati kwa mwaka 2018 makadirio na Kituo cha Kufuatilia Taarifa za Hewa Ukaa imeonesha kuwa kuwango cha ukataji miti kimeongezeka kufikia hekta 469,420.

Misitu na Elimu 

Kama ambavyo kauli mbiu ya Siku ya Kimataifa ya Misitu ya mwaka 2019 inalenga kwenye “Misitu na Elimu”, tunatakiwa kuang’azia umuhimu wa elimu wa misitu katika kukabiliana na changamoto za sasa na baadae. Kwa vipi elimu ya misitu inavojenga maadili, utamaduni na uwajibikaji miongoni mwa watoto wetu katika kutunza na kulinda rasilimali zetu za misitu? Ni kwa kiwango gani mitaala ya elimu inajitosheleza na kwa umuhimu gani kwa sasa kuanzia shule za msingi, secondary na hata taasisi ya elimu ya juu katika kukabiliana na changamoto za sasa na baadae zinazokabili rasilimali za misitu?  Kwa nini idadi ya watu wanaodailiwa ili kusoma masuala ya misitu inapungua kwenye nchi nyingi? Mengi ya haya maswali yanaweza kujibiwa kwa kina huko baadae lakini kwa sasa, hebu tulenge kizazi kichanga.

Kwa muda mrefu elimu imetambuliwa kama njia muhimu ya kushawishi maarifa, mbinu na maadili ya wananchi katika kuunga mkono maendeleo endelevu. Kuwajengea watoto msingi wa kuelewa vyema umuhimu wa misitu ni hatua muhimu katika kuja kulinda rasilimali za asili kwa ajili ya vizazi vijavyo. Kukuza uelewa miongoni mwa watoto wa leo kuhusu matumizi endelevu na utunzwaji bora wa misitu utahamasisha kizazi hiki cha kesho umuhimu wa kufanya maamuzi sahihi juu ya mazingira.

Kuanza kuhamasisha toka utoto

Ni muhimu kuileta elimu ya misitu katika maisha yao katika umri mdogo ili kubadilisha kasumba zilizozoeleka ambazo zinaweka msisitizo katika utunzaji wa misitu kwa kukataza kufanya hili au lile au kutochukua hatua hii au ile. Elimu ya misitu inaweza kuwahamasisha watoto wadogo kujifunza kuhusu umuhimu wa misitu na hata kuja kusomea masuala ya misitu; inaweza kusaidia kuwaunganisha na asilia na hivyo kujenga vizazi vya baadae vinavyotambua faida ya miti na misitu na umuhimu wa kuitumia kwa njia endelevu. Watoto watagunudua miti darasani na hata katika shule za masuala ya misitu, katika kutembelea maeneo ya misitu na sehemu za bustani za misitu chini ya uangalizi wa watu wazima, au kwa kujifunza kuhusu upandaji na ukuzaji wa miti katika majiji na bustani.

Katika nchi kama Tanzania ambapo zaidi ya asilimia 40 ya watu wake wana umri chini ya miaka 15, kuwaelimisha watoto umuhimu wa utunzwaji na utumiaji endelevu wa misitu kama njia ya kimkakati ya kuhakikisha uwajibikaji wa kiikolojia kwa muda mrefu ujao.

Misitu bora ni muhimu katika nia yetu ya kutimiza Malengo ya Maendeleo Endelevu.

* Mwandishi wa Makala hii ni Mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) hapa Tanzania.