FAO.org

Home > Country_collector > FAO in Tanzania > News > Detail
FAO in Tanzania

Ubia ni muhimu kwa ajili ya misitu endelevu

01/04/2019

Mwaka 2012 Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulitangaza Machi 21 kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Misitu. Dunia huadhimisha siku hii kwa kukuza uelewa wa umuhimu wa aina zote za misitu na kukabiliana na baadhi ya changamoto kubwa tulizo nazo kwa sasa, kama vile mabadiliko ya tabia nchi, njaa, umaskini na ongezeko la watu mijini. Misitu itakuwa muhimu zaidi wakati huu ambapo idadi ya watu inapanda kufikia watu bilioni 8.5 ifikapo 2030.

Tamko la Umoja wa Mataifa linaiomba Sekretarieti ya Jumuiko la Umoja wa Mataifa juu ya Misitu (UNFF), kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kufanikisha utekelezaji wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Misitu, kwa kushirikiana na Serikali, Ubia wa Kushirikiana katika Masuala ya Misitu pamoja na taasisi na michakato ya kimataifa, kanda nahata katika Makundi muhimu.

Kauli mbiu iliyochaguliwa kwa mwaka 2019 kwa kushirikiana na wabia katika Masuala ya Misitu: ‘Misitu na Elimu’ ikiwa inalenga kutukumbusha yafuatayo:

Uwekezaji katika elimu ya misitu ni muhimu katika ngazi zote, ili kuendeleza kada ya wataalam, watunga sera, na jamii kusitisha ukataji wa miti na kurudisha maeneo yalizopoteza hadhi yake kutokana na ukataji miti hovyo. Misitu bora inatusaidia kufikia mengo ya Malengo ya Maendeleo Endelevu, kwa mfano kuboresha maisha ya jamii za watu masikini kabisa duniani na kutunza bayonuai.

Nchi nyingi zinajitahidi kuhakikisha kuwa wanawake zaidi wanaingia katika kozi zinazohusiana na masuala ya misitu, kuweka kipaumbele kwenye usawa wa kufikia elimu ya misiti kwa wote. Uwiano wa kijinsia katika elimu ya misitu unawajengea uwezo kina mama wa vijijini wa kutunza misitu kwa njia endelevu.

Wataalamu wa misitu wanatakiwa kujua vyema mambo ya uasilia, pia wajifunze kuhusu teknolojia za kisasa kuhakikisha kuwa misitu yetu inafuatiliwa na kutumika kwa njia endelevu. Jamii za vijijini na zile za asili wana uzoefu wa kutosha na maarifa katika kulinda rasilimali za misitu na kuhakikisha uvunwaji wake endelevu. Wanaweza kurithisha hayo maarifa yao na uzoefu wa vitendo kutoka kizazi kimoja hadi kingine. 

Kuwasaidia watoto kujiunganisha na ulimwengu wa asili kunapelekea kujitambua kwa vizazi vijavyo juu ya faida za miti na misitu na umuhimu wa kuitunza kwa njia endelevu. Kwa baadhi ya watoto, misitu ni chanzo cha moja kwa moja cha chakula, kuni na makazi, na sehemu ya maisha yao ya kila siku. Baadhi ya watoto watagundua misitu wakiwa madarasani au katika shule zilizoko msituni, au kutumia muda kutembelea misitu au sehemu za kupumzikia na kujifunza zaidi juu ya upandaji miti mijini na kwenye bustani.

Katika miongo mine iliyopita ya ubia na ushirikiano na Serikali ya Tanzania, FAO imetoa msaada wa kitaalamu kwa ajili ya utunzwaji endelevu wa misitu hapa nchini kupitia uboreshwaji wa sera ya misitu, mikakati ya kitaifa ya utekelezaji, na mifumo ya kanuni za miongozo mbali mbali; kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya rasilimali za misitu; kujenga uwezo wa wataalam wa misiti na pia kuhamasisha maarifa zaidi katika sekta ya misitu ili kuhakikisha kuwa matumizi na utunzaji wa rasilimali hizi unakuwa endelevu.

Sekta ya Misitu ya Tanzania ni moja ya mihimili mikuu ya uchumi. Watu wa vijijini na mijini wanategemea rasilimali za misitu kwa ajili ya maisha yao yote au kwa kiasi kikubwa. Misitu inatoa malighafi za ujenzi, nishaji na ajira. Misitu inasaidia maisha ya watu wenyeji katika maeneo yao kwa kuwapa chakula cha mifugo, madawa, chakula, asali, ulinzi wa vyanzo vya maji, na pia huduma nyingine muhimu za kiikolojia.

Pamoja na faida zote hizi na hatua mbali mbali muhimu ambazo serikali imechukua, kiwango cha ukataji miti na kuathiriwa kwa misitu bado kipo katika kiwango cha juu kisichokubalika. Kwa mujibu wa taarifa ya Taifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Rasilimali Misitu Tanzania (NAFORMA) ya mwaka 2015, katika kipindi cha kati yam waka 2009 na 2013 Tanzania Bara (Ukiondoa Zanzibar) ina jumla ya Hekta milioni 48.1 za misitu.

Kiwango cha sasa cha uvunaji ni mita za ujazo milioni 62.3 wakati kinachoruhusiwa ni mita za ujazo milioni 42. 8. Hii inamaanisha kuwa kiwango cha ukataji wa miti kinazidi kile kinachoruhusiwa kwa kila mwaka kwa makadirio ya mita za ujazo milioni 19.5. Maana yake ni kuwa kila mwaka ‘tunakopa’ mita za ujazo milioni 19.5 kutoka kwa wakati ujao na vizazi vijavyo! Tunapoteza zaidi ya hekta 372,000 za misitu kila mwaka, na kiwango hiki kinaendelea kuongezeka.

Uwekezaji wa Sekta Binafsi katika masuala ya misitu umeongeza ufanisi wa viwanda vinavyohusiana na bidhaa za misitu, pamoja na kwamba bado mengi zaidi yanatakiwa kufanyika. Changamoto zinazohusiana na uwezo modogo kutokana na teknolojia zilizopitwa na wakati, uwekezaji mdogo, mitaji duni, kutokuwepo na upatikanaji wa uhakika wa malighafi, kutotumika vyema kwa wataalam wenye mafunzo na udhaifu katika maendeleo ya soko bado zipo.

Kupeleka elimu ya misitu kwa kizazi kichanga

FAO na Serikali ya Tanzania wanamalizia mchakato wa kutekeleza mradi wa kipekee miongoni mwa watoto kati ya miaka 9 na 12 ili kukuza elimu ya misitu na uelewa wa faida za misitu na hitaji la kuitunza katika njia iliyo endelevu.

Leo, zaid ya nusu ya watu duniani wanaishi kwenye maeneo ya mijini. Ifikapo 2050, idadi hii inategemewa kuongezeka hadi asilimia 70. Ongzeko hilo la haraka la watu mijini linaleta changamoto katika masuala ya maendeleo endelevu, hususan katika nchi zinazoendelea.

Matokeo yake, watu wanaendelea kutengwa na mazingira ya asili na hivyo kukosa uelewa kuhusu misitu na faida zake. Ni muhimu kuleta ulelewa kuhusu misitu katika maisha yao katika umri mdogo ili kubadilisha kasumba zilizozoeleka ikiwamo misimamo mikali katika kukataza kufanyika kwa hili au kukatazwa kufanyike kwa lile. Elimu ya mapema inaweza kuwahamasisha watoto wadogo kujifunza kuhusu umuhimu wa misitu na hivyo ikiwezekana waje kusomea utaalamu wa misitu.

Mradi huu, ambao unaendana na kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya Misitu – ‘Misitu na Elimu’, utetengeneza nyenzo za kufundishia na kuanzisha mfumo shirikishi na wa vitendo wa kujifunza miongoni mwa watoto ili kuchochea hamu ndani yao ya kupenda na kutunza misitu.

Nia ni kuwapa maarifa na kuwafanya waelewe zaidi juu ya misitu, matumizi yake endelevu, na mahusiano yake na asilia, kuwajengea uwezo watoa elimu katika jamii katika vyuo vilivyochaguliwa awali kuweza kushiriki na kutengeneza nyenzo za kufundishia zenye ubora wa hali ya juu zitakazotumika kujenga uwezo wa washika dau kupitia mafunzo na mbinu za utekelezaji.

Ubia imara unaohusisha Serikali, Sekta Binafsi, Asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa, taasisi za utafiti na elimu, jamii husika utaenda mbali sana kwa misingi ya maendeleo kwa kubadilisha sekta ya misitu, ili ichangie vyema katika uchumi; kuiwezesha kuleta maendeleo kwa kuhakikisha usalama wa chakula na lishe na pia kutunza zile huduma za kiikolojia.