FAO in Tanzania

Ushirikiano wa Serikali na FAO wawezesha wahanga wa tetemeko la ardhi kusimama kwa miguu yao tena Kagera

Shamba la mihogo chini ya mradi huu
11/12/2018

Wakulima wadogo na wale katika ngazi ya familia, hususan wanawake na vijana vijini, wana mchango mkubwa katika kilimo na uchumi wa vijijini hapa Tanzania, na hususan katika Mkoa wa Kagera.

Wanawake ni wadau muhimu sana katika suala la uhakika wa lishe na chakula, kupitia majukumu yao ya nyumbani, na wamekuwa walengwa wakuu wa msaada wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) katika Mkoa huu.

Hali ilivyokuwa baada ya tetemeko

Baada ya tetemeko kubwa la ardhi kutokea katika Mkoa huu mwaka 2016, Wizara ya Kilimo ikawasilisha ombi la msaada wa kitaalam wa kuweza kuzisaidia jamii na mkoa mzima kuhilimili athari za janga hili na pia kuweza kurejea katika hali ya awali. Mamlaka za Mkoa, kwa ushirikiano na, wakaanzisha mtandao wa shule za mafunzo ya kilimo kama nyenzo ya kutoa mafunzo, kubadilishana uzoefu na maarifa ya kilimo, na kusambaza mbegu bora. Tokea hapo, wakulima wengi wadogo katika vijini 26 villages na mitaa yake katika Wilaya za Bukoba, Missenyi, Kyerwa, na Muleba wamekuwa wakihusishwa kikamilifu katika kuzalisha mbegu bora za nafaka na mapandikizi ya mazao mengine kama mihogo na viazi lishe ili kuboresha uhakika na upatikanaji wa chakula katika kaya na vipato.

Ushirikiano miongoni mwa FAO na Taasisi ya utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera umeleta mafanikio makubwa kwani umeweza kuimarisha kilimo na uzalishaji wa chakula Mkoani humo baada ya tetemeko lile la mwaka 2016.

Zaidi ya mapandikizi bora na yenye usugu dhidi ya magonjwa na wadudu 291,000 ya muhogo pamoja na 553,000 ya viazi lishe vyenye vitamini A na madini chuma kwa wingi na mbegu za bora za migomba 4000 zilisambazwa kwa wakulima. Katika vijiji vingi, pandikizi moja la muhogo linaweza kutoa mihogo zaidi ya 10 kwa wastani kutegemeana na namna ya utunzaji wa shamba, aina ya mbegu na rutuba ya udongo. Kwa maharage yaliyoongezewa madini na viini lishe, kila kilo moja iliweza kuzalisha wastani wa kilo 15, kulingana na vigezo hivyo hivyo hapo juu. Kupitia huduma za Wagani mkoani humo, wakulima waliokuwa wanafanya mafunzo katika shule hizi za kilimo kwa vitendo, walienda na kusambaza mbegu hizi bora pamoja na maarifa kwa wakulima wengine katika maeneo yao ndani nan je ya Mkoa wa Kagera.

Kuimarika kwa hali ya chakula 

Hili limeboresha sana hali ya uhakika wa chakula, lishe bora na pia vipato. Kwa mfano, katika Kijiji cha Nkerenge huko Wilayani Missenyi, Kikundi cha Wanawake cha Tuinuane kiliuza mbegu za muhogo zenye thamani ya Tshs. 450,000/- kwa wakulima wengine msimu uliopita wa kilimo.

Mpaka sasa, mradi unasaidia vikundi 53 vyenye wakulima 1,094 Mkoani humo ambao wamekuwa nguzo kuu ya usambazaji wa mbegu bora kwa wakulima wengine kama ifuatavyo: Vikundi 18 vilisambaza mbegu za muhogo kwa wakulima; Vikundi 20 vilisambaza mbegu za viazi lishe kwa wakulima 444; Vikundi 8 vilisambaza mbegu bora za maharage kwa wakulima 122; na vikundi 7 vilihamasisha ukulima wa migomba kwa wakulima 296. Ongezeko la upatikanaji wa mbegu bora na mapandikizi, eneo lililopo kwenye kilimo mkoani humo linategemewa kuongezeka kwa mara mbili au nne zaidi kwa mazao ya muhogo, viazi lishe na maharage.

Mchango wa FAO unaoendeleo Mkoani Kagera ni kuzisaidia jamii kuunganisha juhudi katika kujenga uwezo wa kuhimili majanga kama vile mabadiliko ya tabia ya nchi, hususan katika kuendeleza kilimo chenye kuhimili mabadiliko ya tabia nchi, kilimo chenye kutilia maanani mazao yenye lishe bora, na kuwezesha kusambaa kwa mbegu bora zenye kuhimili ukame, visumbufu na magonjwa.

Kuimarishwa kwa ushirikiano 

Mpaka leo ushirikiano huu wa FAO, Serikali Mkoani Kagera na Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Maruku umepelekea kuwepo kwa mbegu bora kwa wakulima kwa wakati ndani na nje ya vijiji vilivyo katika eneo la mradi. Ushirikiano huu umewezesha kuwepo kwa aina ya mbegu zilizoboreshwa (mihogo, vizazi na maharage), kuongeza uzalishaji na kujenga uwezo wa kipato wa kaya pamoja na kuhimili athari za majanga. Pia usambaaji wa mbegu bora kwenye maeneo mengi, kuboresha lishe na kuongezeka kwa vipato kupitia uzalishaji na uuzaji wa mbegu kibiashara na kuwahakikishia kipato wanawake na vijana.

Mbinu Bora za Kilimo zinazoendeshwa na wataalam wa kilimo Mkoani Kagera, kwa kiasi kikubwa zimechangia mafanikio haya tunayoyaona leo.