FAO in Tanzania

Serikali, FAO wazindua mradi wa kuratibu umiliki wa ardhi

Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Mohammed Utaly, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo
07/02/2019

Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa (FAO) wamezindua mradi wa Msaada wa Kitaalam wa kukuza uwezo wa wadau katika kuratibu mfumo wa utawala wa ardhi hapa nchini. 

Mradi huu unafuatia ombi la Wizara hiyo kwa ajili ya kusaidia uratibu wa mfumo wa umiliki wa ardhi kwa kutumia Miongozo ya Hiari ya Kuboresha Utawala wa Ardhi , Uvuvi na Misitu hapa nchini. Pia unalenga kusaidia katika kuratibu sera na sekta, kukabiliana na migogoro na kuboresha taarifa juu ya uwekezaji katika ardhi hapa Tanzania.

Umuhimu wa Miongozo hii

FAO iliandaa miongozo hii kwenye muktadha wa usalama wa chakula, kama ilivyopitishwa na Kamati ya Dunia ya Usalama wa Chakula tarehe 11 mwezi Mei mwaka 2012 lengo likiwa kuhamasisha juu ya upatikanaji wa haki za umiliki ardhi, uvuvi na misitu kama njia ya kutokomeza njaa na umaskini, kufanikisha maendeleo endelevu na kutunza mazingira.

Uzinduzi rasmi wa mradi huu umefanyika Wilaya ya Movomero, mkoani Morogoro Mgeni Rasmi akiwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Clifford K. Tandari, Pamoja na Mwakilishi wa FAO hapa Tanzania, Fred Kafeero. Mbali ya Wilaya ya Mvomero, mradi hii pia utatekelezwa katika wilaya za Kilombero, Malinyi, Kilosa na Ulanga ambayo ni maeneo yanayofahamika kwa migogoro ya ardhi hususan baina ya wakulima na wafugaji mara nyingine zikipelekea vifo na uharibufu wa mali na mifugo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bw. Tandari alisema kuwa mradi huo umekuja wakati muafaka ambapo serikali ilikuwa inapitia sera na miongozo mbali mbali ikiwemo Sera ya Ardhi katika kuboresha suala la utawala wa ardhi hapa nchini pamoja na kutatua migogoro ya ardhi hapa nchini. “Watu wanategemea kwenye upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji, uvuvi na misitu kwa ajili ya maisha yao. Namna rasilimali hizi zinavyotumika ina athari ya moja kwa moja kwenye uhakika wa chakula, maendeleo vijijini, ukuaji wa uchumi na utunzaji endelevu wa mazingira,” alisema na kuongeza: “Mifumo bora ya umiliki wa ardhi itasaidia kuweka miongozo wa namna kuratibu watu, jamii na wengine katika kufikia rasilimali za asili, kwa kutumia njia rasmi na zisizorasmi na hivyo kuepusha migogoro.”

Bw. Tandari ameipongeza FAO kwa msaada wake kupitia uandaaji wa miongozo hiyo akisema kuwa ni muhimu sana katika kuelekeza juhudi za serikali katika kuandaa programu, sera na kuhakikisha usalama wa chakula.

Kusaidia kutatua changamoto

Kwa upande wake, Bw. Kafeero alisema kuwa miongozo hiyo ni muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa haki wa rasilimali za asili, ambao ni nguzo kuu ya usalama wa chakula na maendeleo. “Kwa sasa tunakabiliwa na changamoto mbali mbali kutokana na ongezeko la watu, ukataji miti, kushuka kwa mazao ya uvuvi, mabadiliko ya tabia nchi na nyingine nyingi. Hizi zote zinaweka mazingira mazuri kwa ajili migogoro juu ya matumizi na umiliki wa rasilimaji, shughuli haramu na uharibifu wa mazingira,” alibainisha. Mwakilishi wa FAO alitahadharisha kuwa bila uwepo wa uwazi juu ya nani anatumia, anadhibiti na kumiliki rasilimali watu walio kwenye mazingira magumu watakuwa katika hatari ya kuwa maskini zaidi na wasio na uhakika wa chakula.

Uzinduzi huu ulihudhuriwa na maafisa kutoka serikali kuu na serikali za mitaa ikijumuisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Raisi TAMISEMI, Mkoa wa Morogoro, Kamisheni ya Matumizi ya Ardhi na Wilaya ya Mvomero, miongoni mwa wengine.